MKUKUTA ni neno maarufu katika jamii ya Tanzania
toka ulipozinduliwa mwaka 2005. Kirefu chake ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini Tanzania , MKUKUTA umeboreshwa
kutoka katika Mkakati wa kwanza wa kupunguza umaskini wa uliozinduliwa Oktoba
mwaka 2000 na unatekelezwa kuanzia 2005 hadi 2010.
Mojawapo ya eneo ambalo MKUKUTA umejikita ni ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa
kipato. Eneo hili lina malengo sita likiwemo la kupunguza umaskini wa kipato
kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini. Inadhamiriwa ifikapo 2010
wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wapungue toka asilimia 38.6 hadi asilimia
14.
Kupungua huko kutatokana na wakazi wa maeneo
hayo ambao wengi wao ni wakulima wadogo vijijini endapo watajengewa uwezo wa
kuongeza tija na kupata faida ndani na nje ya sekta ya kilimo. Kuwezesha
kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo. Kuwajengea uwezo wa kuongeza
thamani mazao wazalishayo ili waweze kupata faida.
Wakazi wa sehemu hizo wajengewe pia uwezo wa
kutumia raslimali zinazowazunguka na hivyo Kuongeza michango inayotokana na
wanyama pori , misitu
na uvuvi katika vipato vya jumuiya za vijijini. Haya yakitekelezwa vyema itakuwa
ni rahisi kwa wakazi hao wa vijijini kupunguza umasikini wa kipato na hivyo
kukuza uchumi.
Tangu MKUKUTA uanze kutekelezwa kumekuwepo
na jitihada mbalimbali za wadau katika utekelezaji wake. Wananchi kila mahali
wameanzisha vyama vya kukopa na kuweka (SACCOS). Vyama hivi vinawasaidia wananchi
wenye kipato cha chini kupata mikopo inayowasaidia kuendeleza kilimo au biashara
zao ndogo ndogo.
Takwimu zilizopatikana zinaonesha hadi mwaka
2007 karibu wajasiriamali wadogo wadogo 20.000 walipatiwa mikopo kutoka kwenye SACCOS
mbalimbali nchini ongezeko zaidi linatarajiwa baada ya hatua ya serikali kutoa
karibu bilioni moja kwa Mkoa ili kusaidia kuwakopesha wanyonge wasioweza
kukopesheka na mabenki.
Kwa muda mrefu kilimo kimekuwa kinakabiliwa na chanagamoto nyingi. Kasi ya kukua
kwa kilimo ni asilimi 5 katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo. Hii inatoa picha inayobashiri kuimarika
zaidi sekta hii iwapo mipango iliyopo itatekelezwa na kusimamiwa vizuri. Basi
wakazi hao wa vijijini wanaweza kuondokana na umaskini.
Kwa upande mwingine, pato la taifa(GDP)
linaendelea kuongezeka. Hii inaashiria uchumi wa nchi kukua. Mfano, mwaka 2006
Pato la taifa lilikuwa kwa asilimia 6.2. Lengo la MKUKUTA linasema ifikapo mwaka
2010 pato hilo
liongezeke na kufikia asilimia kati ya
sita ana nane.
Kumekuwepo
na ongezeko la mapato ya wakazi wa vijijini katika sekta ya ufugaji. Ingawaje
bado wafugaji wanafuga kizamani na kuuza mifugo yao
bila ya kuongeza thamani, bado ng’ombe waliouzwa nje walifikia thamani ya
shilingi za Tanzania
bilioni 2.9 kiasi ambacho ni kikubwa na kinachangia kupunguza umaskini wa
kipato vijijini.
Moja ya vikwazo kufikia lengo hili ni miundombinu, katika maeneo
ya vijijini hasa barabara na umeme ni kiwazo kikubwa cha juhudi za kujikwamua
kiuchumi kwa wakazi wengi wa huko. Barabara zisizounganika zinakwaza usafirishaji
wa mazao na kupata tija kwa wakati muafaka. Mazao mengi huozea mashambani hasa
wakati wa msimu wa matunda
Umaskini wa kipato
vijijini unachangiwa na wakulima kuendesha kilimo cha kujikimu kwa kutegemea
mvua, uzalishaji duni, nguvu kazi haba na vitendea kazi duni ingawaje huduma za
kilimo cha umwagiliaji zinaonesha kuanza kukua lakini wananchi wengi hawatumii
kutokana na ubunifu mdogo na baadhi ya wanaotumia wamefanikiwa.
Mitaji na fursa finyu ya kupata mikopo ni changamoto
kwa wakazi wengi wa vijijini. Maeneo ya mijini tatizo linaonekana sio kubwa sana ukilinganisha na
maeneo ya vijijini. Ndio maana MKUKUTA umeyatenga malengo ya kupunguza umaskini
wa kipato kwa wakazi wa mijini tofauti na wale wa vijijini kwa vile wanahitaji
mbinu tofauti.
Matumizi halisi ya nishati ya kupikia ni
changamoto kwa wengi. Serikali inasisitiza nishati za umeme na gesi zitumike
hasa ili kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ya kuni. Kwa wakazi wengi
wa vijijini hili bado ni tatizo. Kutokana na gharama za nishati mbadala wengi
hawaziwezi huendelea kutumia kuni na mkaa.
Hali ngumu ya maisha hasa umaskini wa kipato
kwa mtu mmoja mmoja unaripotiwa kuongezeka hasa mwaka 2007. Karibu asilimia 82
ya vijana waliosailiwa katika zoezi la kukusanya maoni ya wananchi juu ya
MKUKUTA walidai ugumu wa maisha unaongezeka kila siku kutokana na kukosa ajira
na kupanda kwa garama za maisha.
Serikali licha ya
kuwa na mikakati ya kuboresha miundombinu ya kiuchumi kama
vile barabara, huduma za umeme na maji maeneo ya vijijini, ili kuchagiza
maendeleo katika maeneo mengi ya nchi hasa vijijini, mikakati hiyo iende
sambamba na upatikanaji wa nishati za uhakika na hasa umeme wa jua ambao
utachangia kupunguza kazi za sulba.
Viongozi wanapaswa
kuhamasisha wakulima vijijini kuzalisha mazao yenye faida kubwa na kuongeza
upatikanaji wa nyenzo za kilimo na matumizi sahihi ya teknolojia Suala hili
liende sanjari na mbinu za usimamizi wa mavuno katika kaya za vijijini na
kukuza miradi inayoongeza thamani katika kilimo,uvuvi mifugo na bidhaa za
misituni
Katika lengo hili
kuna mikakati kundi zaidi ya kumi na nane iwapo serikali na wadau watahakikisha
mikakati kundi hiyo inatekelezwa haraka wananchi wa vijijini wake kwa waume
wanaweza kupunguza umaskini wa kipato na kuvigeuza vijiji kuwa kimbilio la watu
wengi kuliko ilivyo hivi sasa vijana huvikimbia kuogopa kuzama kwenye umaskini.
Yapo maeneo ambayo
wananchi wake hawahitaji fedha kwa ajili ya mitaji ya kuongeza kipato lakini
wanakabiliwa na umaskini wa kipato kutokana na sheria ambazo kama zingerekebishwa
zingeweza kuwajengea mazingira mazuri ya kuinua hali za maisha yao Ni jukumu la
serikali kupitia sheria zenye mapungufu
na kuziboresha ili kuleta mafanikio katika kuleta maendeleo kwa taifa.
Mungu ibariki Tanzania
No comments:
Post a Comment